Prof Sifuni Mchome
Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania imetangaza kufuta daraja sifuri katika
matokeo ya elimu ya sekondari nchini na kuongeza daraja la tano ambapo
pia matokeo ya kidato cha nne kwa watahiniwa wanaorudia mitihani
yatahusisha matokeo yao ya awali wakati wakiwa shuleni ili
kuwarahisishia kupata alama nzuri.
Katibu mkuu wa Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi Profesa Sifuni
Mchome amesema pamoja na marekebisho hayo pia wameongeza daraja B ya juu
(B+) kwa alama za ufaulu ambapo daraja A kiwango cha ufaulu ni kati ya alama 75
na 100, daraja B la juu (B+) ni kati ya alama 60 na 74, daraja B la kati (B) ni
50 na 59, daraja C kati ya 40 na 49, daraja D kati ya 30 na 39, daraja E
kati ya 20 na 29 na daraja F ni kati ya alama 0 na 19.
Profesa Mchome amesema marekebisho hayo yanalenga kuinua kiwango na
kuboresha kiwango cha elimu Tanzania ambapo kwa kila mhitimu wa kidato
cha nne matokeo yake ya mwisho yatachangia alama 60 yatajumlishwa na alama 40
ambazo zitatokana na majibu ya mitihani ya kidato cha pili, cha tatu na
mtihani wa Mock.
“Alama A itakuwa ni ufaulu uliojipambanua, B+ itakuwa ni ufaulu bora
sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu mzuri, D ufaulu hafifu, E ufaulu
hafifu sana na F ufaulu usioridhisha kabisa,” alisema Profesa Mchome.
Aliongeza pia kwa kusema kuwa, utaratibu wa sasa wa kupanga matokeo hayo kwa madaraja, utabadilika muda wowote kuanzia sasa na kwamba utakaokuwa ukitumika ni ule wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Point Average ‘GPA’).
Mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka huu
utafanyika November 4, 2013 ambapo zaidi ya Watahiniwa laki nne
wanatarajiwa kufanya mtihani hii ambapo kati yao, Watahiniwa laki 3 na
elfu 67,399 ni kutoka shuleni huku Wavulana ni 198,257 sawa na asilimia
53.69 na Wasichana ni 169,142 sawa na asilimia 46.04 ambapo vituo vya
kufanyia mitihani ni 4,365.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !