WAMO STEVEN KANUMBA, AMINA CHIFUPA, JAMES DANDU, MAFISANGO, COPLEX NA SHARO MILONEA, AJALI ZAONGOZA KUWAPOTEZA
Vifo vya nyota hao licha ya kuacha mapengo
yasiyozibika, bado vimeendelea kugonga vichwa vya watu, vikiacha maswali
na pengine yatima katika familia zao.
Katika makala haya mwandishi wetu amejaribu
kuainisha baadhi ya wasanii wa fani tofauti, waliofariki kipindi ambacho
nyota zao ziking’ara na kupendwa na mashabiki.
SHARO MILONEA
Namna ya
uigizaji wake katika hali ya kitanashati na mikogo ya kipekee
inayoendana na lugha ya ‘kisharobaro’, ilimfanya msanii huyo kupoteza
jina lake halisi ambalo ni Husseni Ramadhani Mkieti.
Ilikuwa vigumu
kumsaka msanii huyo kwa jina lake halisi, lakini ilikuwa ni rahisi
kumpata iwapo ungemtafuta kwa jina la Sharo Milionea.
Msani huyo alibadilisha jina lake la awali na
Sharobaro na kuwa Sharo Milionea, baada ya kuingia mzozo na msanii
mwenzake, Bob Junior ambapo kwa kuepusha wasikosane, aliamua kutumia
jina hilo jipya lililokolea na kumvaa kuliko maelezo.
Katika mahojiano mbali mbali Sharo Milionea
aliwahi kunukuliwa akisema kuwa alipenda kuigiza kama brazameni akitumia
maneno kama 'usinichafue meen', 'nimechoka kuimba meen' kamata 'mwizi
meen' ili kujitofautisha na wasanii wengine nchini, akiiga staili ya
msanii aliyekuwa akimhusudu, Will Smith.
Sharo Milionea, aliyekuwa mahiri kwa kuigiza
filamu na uimbaji wa muziki wa kizazi kipya, alikiri kwamba karibu kila
jambo katika sanaa yake, ina chembe ya nyota huyo wa Kimarekani
anayetamba kwenye muziki na filamu ulimwenguni.
Mkali huyo aliyewahi kutamba na nyimbo kama
'Nahesabu Namba','Tusigombane', 'Chuki Bure', 'Hawataki', 'Sondela',
'Tembea Kisharobaro' ambaye pia alikuwa mbioni kuachia nyimbo nyingine
za 'Vululuvululu' na 'Changanyachanganya', amefariki Jumatatu ya Novemba
26 saa mbili usiku maeneo ya Maguzoni Muheza mkoani Tanga kwa ajali ya
gari akitokea Dar es Salaam.
AMINA CHIFUPA
Nyota huyu
alizaliwa Mei 20 mwaka 1981 na kufariki Juni 26 Juni, 2007 baada ya
kuugua. Kifo chake kilitokea siku chache kabla ya kikao cha Bunge la
Bajeti, akiwa mbunge.
Chifupa alipata umaarufu wa kuwa Mbunge kijana
mwenye umri mdogo ambapo alitikisa kwa kula kiapo mbele ya Bunge
katika harakati za kuwamata wauza na watumiaji wa madawa ya kulevya.
Ndani ya miezi 18 alishikilia bango msemo wake wa kutetea vijana, kupunguza rushwa na pia elimu kwa watu wote.
Kabla ya hapo alikuwa ni mtangazaji maarufu wa redio ya Clouds FM.
JAMES DANDU
Maarufu kama 'Cool James', Mtoto wa Dandu Mwanamuziki aliyezaliwa 1970 katika Jiji la Mwanza.
Alianza shughuli za muziki mwaka 1983, lakini
album yake ya kwanza aliitoa 1986. Alijiunga na mwanamuziki Andrew
Muturi kutoka Kenya na kuanzisha kundi la Swahili Nation ambapo
walifanikiwa kutoa single iliyoitwa Mapenzi.
Mwaka 1990 alijitoa kundi hilo na kuanzisha kampuni yake Dandu
Planet Mwaka 1993 akiwa na Black Teacher. Alianzisha kampuni nyingine
Dandu Entertainment na kufanya kazi kadhaa kupitia wanamuziki wa Afrika
Mashariki.
Dandu hatasahaulika kwa wale wanaofahamu chanzo
cha tuzo za kila mwaka za muziki za Kilimanjaro Music Awards ambazo
zilianza kwa jina la Tanzania Music Awards (TAMA).
Alifariki katika
ajali ya gari tarehe 27 Agosti 2002 akiwa na umri wa miaka 32 huku kibao
chake cha 'Mtoto wa Dandu' kikishika chati ya juu vituo mbali mbali vya
radio.
ISSA KIJOTI
Nyota yake ilizima ghafla kufuatia ajali ya gari
iliyogharimu maisha yake na wasanii wenzake, iliyotokea Machi 21 mwaka
2011, maeneo ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, mkoani Morogoro.
Kijoti alipoteza maisha pamoja na wasani wengine 13 wa kundi la Five Stars tukio ambalo litabaki kuwa historia.
Kijoti
alifariki akiwa na umri wa miaka 26 wakati nyota yake inang'aa hasa
baada ya kupata umaarufu mkubwa akiwa na kundi hilo baada ya kutoa kibao
cha 'Wapambe Msitujadili'.
STEVE KANUMBA
Aprili 10 mwaka huu, Tanzania ilimpoteza mmoja wa wasanii wake mahiri katika tasnia ya filamu, Steven Kanumba.
Kanumba
alifariki alfajiri ya Jumamosi Aprili 7, akiwa na umri wa miaka 28,
baada ya kile kilichodaiwa kuwa ugomvi wa kimapenzi na rafiki yake wa
kike, ambaye pia ni mwigizaji, anayefahamika kwa jina Elizabeth Michael,
maarufu ‘Lulu’.
Umati wa watu wakiwamo Rais Jakaya Kikwete,
maoafisa waandamizi wa Serikali, wasanii na watu wa tabaka mbambali
walihudhuria msiba huo, ambapo pia walikusanyika katika viwanja vya
Leader’s kutoa heshima zao za mwisho kabla ya mazishi yaliyofanyika
makaburi ya Kinondoni.
Idadi hiyo kubwa inayoingia katika rekodi za pekee
ni ya pili kutokea baada ya umati uliofurika wakati wa kuaga mwili wa
Baba wa Taifa, Mwalimu Julias Kambarage Nyerere.
Huo ni ushahidi
tosha wa umaarufu mkubwa aliokuwa nao Kanumba, ambaye hadi mauti
yalipomkuta aliweza kutengeneza zaidi ya filamu 40 akishirikiana na
wasanii mbali mbali ndani na nje ya nchi na hasa Nigeria.
PATRICK MAFISANGO
Alikuwa
mchezaji wa klabu ya Simba ya Jijini Dar es Salaam, aliyezaliwa Machi
tisa mwaka 1980 na kufariki Mei 17 mwaka 2012 kwa ajali ya gari
iliyotokea maeneo ya Tanzara, alipokuwa akijaribu kumkwepa mwendesha
pikipiki, ambapo gari lake lilipoteza mwelekeo, kuacha njia na
kutumbukia mtaroni na kugharimu maisha ya mchezaji huyo, ambaye pengo
lake hadi sasa Simba wameshindwa kuliziba.
Mafisango aliagwa kwenye viwanja vya Chang'ombe na kwenda kuzikwa kwenye Kijiji cha Lembe Kinshansa nchini Kongo.
Kifo chake kiliacha taaruki kubwa hasa kwa wapenzi
wa soka kwani alikuwa ni mchezaji wa aina yake Simba, hakuwahi kuwa
nahodha wa timu kama kwenye timu yake ya APR ya Rwanda na Amavubi,
lakini alikuwa ni zaidi ya nahodha kwani aliweza kuhamasisha wenzake
kucheza bila kuchoka na kutokata tamaa hata pale Simba inaposhambuliwa
na timu pinzani na au hata kufungwa.
VIVIAN NA COMPLEX
Ilikuwa ni
saa tatu asubuhi ya Jumapili, Agosti 21 mwaka 2005 ambapo nyota wawili
wa muziki nchini waliokuwa wakipendwa sana, Saimon Sayi maarufu kama
Complex ambaye kipindi hicho alikuwa akifanya kazi na studio ya Aigies
Records na mtangazaji wa Clouds FM na rapper Vivian Tillya walipofariki
kwa ajali ya gari eneo la Mbwewe, mkoani Tanga.
Wasanii hao ambao walikuwa wapenzi, walikuwa safarini kutoka
Morogoro kwenye tamasha la Fiesta iliyopewa jina la ‘Moto Zaidi’
wakielekea jijini Arusha kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya ndoa ya
wazazi wa Vivian.
Siku hiyo pia Vivian alikuwa akienda kumtabulisha Complex kama mchumba wake kwa wazazi wake.
STEVE 2K
Alitamba na kundi la
Mambo Poa, ambalo lilikuwa likisifika zaidi kwa kuimba nyimbo zake kwa
mtindo wa mduara, rap, zouk na raga. Kundi hilo lilikuwa likiundwa na
wasanii Steven Waymark ‘Steve 2K’, John Mjema wote ni marehemu pamoja na
Rashid Mustafa ‘Spider’.
Kupitia nyimbo za wasanii hao kama ‘Shani’,
‘Mimi Siyo Mwizi’, ‘Nilikupenda’, ‘Spare Tyre’, ‘Kasuku’, ‘Mama Afrika’
na nyinginezo, kundi hilo lililoanzishwa mwishoni mwa miaka ya 1990,
liliweza kujipatia umaarufu mkubwa nchini.
Steve 2K aliuawa kwa kuchomwa kisu na
mtayarishaji, Castol mwaka 2004 baada ya kilichoelezwa kuwa ni
kutofautiama, hivyo kuzima nyota ya msanii huyo ambayo kwa wakati huo
iking'aa.
Mwaka 2008, msanii mwingine, John Mjema naye
alipoteza maisha baada ya kujinyonga huku sababu za kitendo hicho zikiwa
kitendawili bado.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !