Madini ya Tanzanite |
HATIMAYE Serikali imeamua kuvunja ukimya
na kutoa uamuzi kuhusu sakata la umiliki wa hisa za mgodi wa madini wa
Tanzanite One uliopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara na kuamuru
wananchi pamoja na kampuni hiyo kugawana “pasu kwa pasu” asilimia 50
kila mmoja.
Hatua hiyo imekuja baada ya mvutano mkubwa kuibuka
kuhusu umiliki wa mgodi huo kufuatia wachimbaji wadogo kutaka wapewe
asilimia 50 kuchimba madini hayo ya vito huku sheria mpya ya madini
ikiwabana wawekezaji hao kutochimba madini hayo ya vito kwa asilimia 100
isipokuwa si zaidi ya asilimia 50 tu.
Hata hivyo,itakumbukwa ya kuwa,Rais Jakaya Kikwete
aliwahi kutoa ahadi katika kijiji cha Lengast wilayani Simanjiro mkoani
humo wakati akijinadi katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010 kwamba
angemegea wachimbaji wadogo eneo la mgodi huo mara baada ya wawekezaji
hao kumaliza mkataba wao ulioisha mwezi machi mwaka huu. Akizungumza
katika mkutano wa kumpokea na kumkaribisha nyumbani Katibu Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi(CCM),Abdulrahamn Kinana, Waziri wa Nishati na
Madini,Sospeter Muhongo alitamka kuwa hivi karibuni suluhisho
litapatikana ambapo wawekezaji hao watamiliki asilimia 50 na wachimbaji
watapewa asilimia 50.
Waziri huyo alienda mbali zaidi na kusisitiza ya
kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kumiliki asilimia 60 katika mgodi
huo huku akisema wamejidhatiti kuhakikisha migodi yote inalipa asilimia 4
kama mrabaha.
Naye Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen
Masele alitamka kwamba Serikali itahakikisha Mkoa wa Arusha unakuwa
Kituo cha Kimataifa cha Madini ya Vito.
Alisema kuwa Serikali iko katika mchakato wa
kuhakikisha kituo hicho kinajengwa hivi karibuni huku akiwaonya wale
watakaowawekea vikwazo vijana wanaofanya biashara ya vito vya madini
hususani ya Tanzanite.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !