Habari Zetu :

Home » , » WABUNGE SASA PINGU KAMA RAIA WENGINE

WABUNGE SASA PINGU KAMA RAIA WENGINE

Written By Unknown on Thursday, November 29, 2012 | 12:59 PM

                                             David Kafulila
Wabunge wa Mkoa wa Kigoma wamemtunishia misuli Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Mstaafu Issa Machibya, kutokana na kuwatishia kuwafunga pingu kama raia wengine wa kawaida, wakisema kauli hiyo ni dharau kubwa kwao wakiwa ni moja ya mihimili mitatu ya dola wenye jukumu la kuishauri na kuisimamia serikali, hivyo anapaswa kuwaomba radhi.
Kanali Machibya anadaiwa kutoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, katika kongamano la uwekezaji Kanda ya Ziwa Tanganyika, mkoani Katavi, kwa kutamka kwamba, mbunge yeyote atakayekaidi maelekezo yake au maelekezo ya mkuu wa wilaya atakamatwa na kupigwa pingu kama raia wengine wa kawaida.
Wakuu wa mikoa mitatu inayounda ukanda huo, ambayo ni Kigoma, Katavi na Rukwa, walihudhuria kongamano hilo pamoja na wakuu wa wilaya na watendaji wengine, wakiwamo makatibu tawala wa mikoa (RAS)na wilaya (DAS).
MOSES MACHALI
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, alisema jana kuwa kwa kauli hiyo, Kanali Machibya ameonyesha kuwadharau wabunge kwamba, ni watu wasiofikiria.
“Kwa hiyo, tunamtaka ombe radhi. Aelewe kwamba, tunafanya kazi zetu kwa mujibu wa sheria. Hivyo, anapaswa aheshimu mhimili wa wabunge,” alisema Machali.
Alisema kauli hiyo ya Machibya ni ya kipuuzi na pia ni ya kifedhuli uliopindukia kwani imeonyesha mkuu huyo wa mkoa ana uwezo mdogo wa kufikiri kinyume cha ulimwengu wa sasa ulivyo.
Machali alisema Machibya anasahau kuwa yeye si bosi wa wabunge na kwa hiyo, hawezi kumfunga mbunge yeyote pingu kama anavyotamba.
Alisema kama itatokea mbunge akampinga mkuu wa mkoa, basi atakuwa ana sababu za msingi za kufanya hivyo.
Pia, alisema elimu ambayo ameipata itakuwa haijamsaidia kitu kama hatapingana na ufisadi kama ule uliopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma na haitakuwa haki kama mkuu wa mkoa atathubutu kumfunga pingu kwa sababu tu ya kupingana na maovu hayo.
“Ibara ya 63 ya Katiba ya nchi inaeleza kuwa kazi ya wabunge ni kuishauri na kuisimamia serikali. Kwa maana hiyo, sisi ndiyo wasimamizi wake (mkuu wa mkoa), lazima afahamu hivyo. Sasa huu ujasiri wa kutamka aliyoyatamka sijui anautoa wapi?” alihoji Machali.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Kanali Machibya hana ubavu wa kuwafunga wabunge pingu na kusema kama atathubutu kufanya hivyo, basi yeye na polisi watakuwa ni wapuuzi na mafisadi.
“Kwanza kuna watu wengine huwa hatutishwi. Bungeni tunampinga waziri, na waziri hawezi kuagiza nifungwe pingu. Sasa kwa kauli yake hiyo, nampinga Machibya. Aje kunikamata,” alisema Machali.

FELIX MKOSAMALI
Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, alisema kauli hiyo ya Kanali Machibya inaonyesha kuwa ana mawazo ya zamani na ya kikoloni kwani anajua fika kuwa yeye ndiye anayepaswa kufuata maelekezo ya wabunge na si wabunge kufuata maelekezo yake.
“Hawezi kuja hapa Kibondo akanielekeza mimi, anielekeza nini? Yeye ndiye aliyenichagua?” alihoji Mkosamali na kuongeza:
“Mkuu wa Mkoa amekosea sana. Mimi naelekezwa na wananchi na sisi wabunge ndiyo tunaomsimamia yeye. Tunakagua hadi Ofisi ya Rais. Hivyo, (Machibya) hana mamlaka hayo. Hizo ni ndoto.”

PETER SERUKAMBA
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, alisema Kanali Machibya amejisikia kutoa kauli hiyo kwani hadhani kama anaweza kuitekeleza kwa vitendo.
“Alikuwa anafurahisha genge tu. Aliwahi kuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Mara na sasa Kigoma, je, aliwahi kumfunga pingu nani? Kama huo ni mpango wake mpya, basi tunamtakia kila kheri katika huo mpango wake mpya,” alisema Serukamba.
ZITTO KABWE
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alisema haamini kama Kanali Machibya anaweza kutoa kauli hiyo.
“Nachelea kutoa kauli mpaka nitakapowasiliana naye (Kanali Machibya) kujua ana maana gani,” alisema Zitto.
Alisema anasita kuto kauli kwa sasa kwa kuwa wabunge wa Mkoa wa Kigoma pamoja na Kanali Machibya wamekuwa wakishirikiana na kufanya kazi vizuri na kusema: “Inawezekana aliteleza au ametafsiriwa vibaya.”
DAVID KAFULILA
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema kwa mujibu wa sheria, kinga na madaraka ya Bunge, hairuhusiwi kumkamata mbunge katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge bila ridhaa ya Spika wa Bunge.
“Hivyo, kauli ya Kanali Machibya inaonesha kuchoka kwake. Haya ndiyo madhara ya kuteua wastaafu kuwa wakuu wa mikoa na wilaya,” alisema Kafulila.
Kanali Machibya anadaiwa kutoa kauli hiyo baada ya Waziri Mkuu kusisitiza katika kongamano hilo uhusiano mzuri baina ya wakuu wa mikoa, wilaya na wabunge.
Kanali Machibya alitoa kauli hiyo, baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Venace Mwamoto, kulalamika kuhusu mivutano aliyonayo baina yake na Mkosamali.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

PROFESSIONAL BLOG DESIGNERS

PROFESSIONAL BLOG DESIGNERS

IDADI YA WATU

BLOG ARCHIVE

DROP YOUR COMMENTS HERE

 
Designed by : Bongo Blogs Designers | Bloggerized by | Tryphone Chasama Jr
Contacts: 0719 625003 / 0765 860437Welcome
Copyright © 2011. SNOUT HOT NEWZ - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template