ARV'S BANDIA ZIMETENGENEZWA TPI:SERIKALI IMESEMA
Naibu Waziri Mh.Dkt Rashid akiwapungia mikono kuwasalimia watumishi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
|
|
|
LICHA ya wamiliki wa kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical
Industries Limited (TPI) kukana kutengeneza na kusambaza dawa bandia za
kupunguza makali ya ukimwi, serikali imethibitisha kuwa kiwanda hicho
ndicho kilitengeneza dawa hizo aina ya TT-VIR 30 yenye toleo Na
OC.01.85.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk. Seif Rashid, akisema kuwa serikali itawachukuliwa hatua za
kisheria wote waliohusika katika suala hilo.
Alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa suala hilo hatari linapatiwa
ufumbuzi wa kudumu na kuzuia lisitokee tena, kabla ya kuchukua hatua
hizo za kisheria uchunguzi unafanywa kupitia vyombo vya usalama.
Dk. Rashid alikiri kuingia katika mzunguko kwa dawa hizo bandia lakini
akawatoa hofu wagonjwa wote wanaotumia (ARV’s) kuwa dawa zinazopatikana
kwenye vituo vya kutolea huduma hiyo kwa sasa ni salama na zenye
viwango vinavyotakiwa.
“Tunatoa wito kwamba waendelee kutumia dawa hizo kama wanavyoshauriwa
na madaktari… kupitia Wizara ya Afya, serikali imehakikisha uwepo wa
dawa za kutosha na kupunguza makali ya ukimwi katika vituo vyote vya
kutolea huduma za afya,” alisema.
Dk. Rashid alifafanua kuwa Wizara ya Afya hununua dawa hizo kupitia
Bohari ya Dawa (MSD), ambayo imepewa jukumu la kununua, kuzitunza na
kusambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Alisema kwa hapa nchini kuna kiwanda kimoja tu cha TPI
kinachotengeneza dawa hizo na kwamba zile za bandia zilibainika mwanzoni
mwa Agosti mwaka huu katika ukaguzi wa kawaida wa Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA) katika Hospitali ya Tarime.
Alisema baada ya ukaguzi na uchunguzi kwenye vituo vyote vya huduma za
afya katika mkoa wa Mara na nchi nzima ilibainika kuwa dawa yenye jina
la biashara TT-VIR 30 toleo namba 0C.01.85 ni bandia.
Alisema pia ilibainika kuwa nyaraka zilizokutwa katika Bohari ya Dawa
(MSD) zinaonyesha kuwa TPI iliiuzia MSD dawa hiyo bandia toleo namba
0C.01.85.
Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa uchunguzi ulibaini kuwa dawa hiyo
bandia ilikuwa na dawa zenye rangi tatu tofauti, njano, nyeupe na
vidonge vya rangi mbili tofauti za pinki na nyeupe.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo wa Afya, dawa zilizokuwa na rangi ya
njano, zilikuwa na kiambata cha Efaverenz badala ya viambata aina ya
Nevirapine, Lamivudine na Stavudine vinavyopaswa kuwemo.
Aidha vidonge vyenye rangi nyeupe na vile vyenye rangi ya pinki na
nyeupe vilikuwa na viambata vinavyotakiwa kuwepo yaani Nevirapine,
Lamivudine na Stavudine kama ilivyokuwa kwenye lebo.
Akielezea kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali baada ya matokeo
hayo ya uchunguzi alisema ni pamoja na kusimamisha mara moja matumizi ya
dawa hizo aina ya TT-VIR 30 toleo Na 0C.01.85.
Hatua nyingine ni pamoja na kusitisha uzalishaji wa dawa zote katika
kiwanda cha TPI Ltd hadi uchunguzi wa suala hilo utakapokamilika ikiwa
ni pamoja na kujiridhisha tena ubora wa dawa inazozalisha.
Alisema pia vigogo wa MSD akiwamo mkurugenzi wake walisimamishwa na
kwamba wizara imeunda timu ya wataalamu kwa lengo la kufuatilia
mwendelezo wa tiba na matunzo kwa wagonjwa wa ukimwi.
Bi. Zarina Madabida akielezea sakata la ARV's
bandia kabla serikali haijatoa msimamo wake.
|
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !